Ijumaa 13 Novemba 2026 - 07:17
Siri ya uumbaji na kiungo kinachounganisha Utume na Uimamu kwa mtazamo wa Ayatullah Wahid Khorasani

Hawza/ Katika ulimwengu mpana wa maarifa ya Bibi Fatimah Zahraa (a.s), fikra bora kabisa za kibinadamu zimeshindwa kuelewa na akili zenye uwezo mkubwa zaidi wa kupaa katika upeo wa fikra zimebaki katika mshangao na mkanganyiko. Kina cha vyeo na hadhi za Bibi huyo kipo nje ya uwezo wa upeo wa uelewa wa mwanadamu, na hakuna kiumbe chochote isipokuwa Maasumu anayeweza kumtambua Maasumu huyo mwanamke. Kwa hiyo, ni lazima kutegemea hazina ya riwaya.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Al-Udhma Wahid Khorasani, katika maandishi yake yanayoeleza fadhila na vyeo vya Bibi Fatimah Zahraa (a.s), amefafanua nafasi yake ya kipekee katika kuunganisha Utume na Uimamu, ukweli wa uumbaji na maarifa ya Qur’ani na Ahlul-Bayt. Aidha, ameeleza baadhi ya madhihirisho ya utukufu wa mwanamke huyo mkuu.

Utangulizi

Kuhusu ukweli wa uwepo na utakatifu wa kiroho wa Bibi Fatimah Zahraa (ambaye rehema na amani ya Mwenyezi Mungu zimshukie), vitabu vingi vimeandikwa na hotuba nyingi zimetolewa juu ya mimbari. Hata hivyo, endapo maandishi na hotuba hizo zingeongezeka mara elfu zaidi, na fikra za mwanadamu zikazalisha maandishi na maelezo mengi zaidi kuhusu jambo hilo, bado yote hayo yasingekuwa chochote zaidi ya tone moja kutoka katika bahari isiyo na mwisho ya fadhila za Bibi Khayrun Nisaa (a.s).

Tunasema nini hasa? Katika ulimwengu mpana wa maarifa ya Bibi Fatimah Zahraa (a.s), fikra bora kabisa za kibinadamu zimeshindwa kuelewa, na akili zenye uwezo mkubwa zaidi wa kupaa katika upeo wa fikra zimebaki katika mshangao na mkanganyiko!

Kwa msingi huo, kina cha vyeo na hadhi za Bibi Fatimah Zahraa (a.s) kipo nje ya upeo wa uelewa wa mwanadamu, na hakuna kiumbe chochote isipokuwa Maasumu anayeweza kumtambua kwa hakika mwanamke huyo Maasumu. Kwa sababu hiyo, daraja lake la juu na nafasi yake tukufu ya kipekee katika uumbaji ni kubwa kiasi kwamba haliwezi kuingia katika upeo wa maarifa ya wanadamu.

Riwaya sahihi pia zinathibitisha ukweli huu kwamba jina lake lilichaguliwa kwa kuzingatia maana hiyo hiyo:

«إِنّمَا سُمِّیتْ فَاطِمَةَ لِأَنَّ الْخلْقَ فطِمُوا عَنْ مَعْرِفَتِهَا»

“Hakika Fatimah aliitwa kwa jina hilo kwa sababu viumbe wamekatishwa na kunyimwa uwezo wa kumfahamu na kumtambua.”

Sasa, ni nani anayeweza kuthubutu kufungua kinywa chake na kudai kwamba mimi nimeufahamu ukweli wa nuru ya Bibi Fatimah Zahraa (a.s)?! Viumbe vyote vilivyomo katika ulimwengu huu, kuanzia viumbe wa ardhini hadi wakazi wa mbinguni, vyote vimeshindwa kutambua kiini cha uwepo wake. Isipokuwa Maasumu (amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao wote), viumbe wote wanajumuishwa katika kauli hii: «فُطِمُوا وَانْقَطَعُوا عَنْ مَعْرِفَتِهَا» — yaani, wamekatishwa na kunyimwa uwezo wa kumfahamu.

Kwa hiyo, tunapaswa kutegemea hazina ya riwaya na kuzungumza kwa kadiri ya kiwango cha maarifa yetu, kama asemavyo mshairi:

“Endapo hutaweza kuchota maji yote ya bahari,
     Basi unywe kwa kadiri ya kiu yako.”

Katika siku hizi, inafaa zaidi kuliko wakati mwingine wowote kuipamba makala yetu kwa maandishi yenye msisimko na mvuto kutoka kwa Marjaa wa Kishia mwenye mapenzi ya dhati kwa Wilaya na mwenye kufahamu siri za mambo, Ayatullah Al-Udhma Wahid Khorasani (Mwenyezi Mungu ampe afya na amkinge na maradhi), ili tujifunze kutoka kwa mwanazuoni huyo mwenye hekima na busara namna ya kuonyesha adabu na heshima mbele ya utukufu mtakatifu wa Bibi Fatimah (a.s).

Huyu ni Marji' ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kuhuisha na kueneza msimu wa Fatimiyyah, na alijitahidi kwa nguvu zake zote kuhuisha alama na nembo za kidini zinazohusiana na Bibi Fatimah (a.s). Katika maandishi haya, kwa kutegemea msingi wa mafundisho ya «Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Ahlul-Bayt wangu», na kwa kutumia kalamu yenye mvuto wa kipekee, amewasilisha fadhila muhimu zaidi za Bibi Fatimah Zahraa (amani iwe juu yake).

Maandishi ya moyoni kuhusu Bibi Fatimah kutoka kwa Marji' mwenye mapenzi ya dhati kwa Wilaya

1. Kiungo kikuu kinachounganisha Utume na Uimamu

Kwa hakika, inaweza kusemwa kwamba kiungo kinachowaunganisha wanachama wote wa Umma huu, kuanzia sasa hadi Siku ya Kiyama, na Utume huo mkuu pamoja na Uimamu huo mkubwa, ni Bibi Fatimah Zahraa (amani iwe juu yake), mwanamke mwenye asili ya kibinadamu lakini mwenye utukufu wa wanawake wa Peponi.

Yeye ndiye njia ambayo kupitia kwake uwepo wa Mtume wa Mwisho unaendelea katika ulimwengu huu. Hii ni kwa sababu upande wake wa kimwili, ambao ni kizazi chake, na upande wake wa kimalaika na kiroho, ambao ni dini yake, vyote vinadumu na kubaki kupitia kwa Siddiqah Kubraa (Bibi Fatimah Zahraa).

Yeye ndiye kiungo kinachowezesha kuchomoza nyota za mbingu ya Uimamu. Upeo wa maisha yake ndio mashariki ya uvumilivu wa Hassan, ushujaa wa Hussein, ibada ya Sajjad, athari tukufu za Baqir, mafundisho ya Jaafar, elimu za Kadhim, hoja za Ridha, ukarimu wa Taqi, usafi na utakatifu wa Naqi, pamoja na haiba na utukufu wa Askari.

Kuanzia kwa Hussein, ambaye ni taa ya uongofu na safina ya wokovu, hadi kwa Mahdi Mtarajiwa, ambaye ndiye mwisho wa urithi wa Manabii, ambaye kwa kupitia kwake viumbe hupata riziki na ambaye kwa uwepo wake ardhi na mbingu hudumu, wote ni matunda ya mti huo mwema ambao mizizi yake imethibiti ardhini, matawi yake yameinuka hadi mbinguni na ambao kwa idhini ya Mola wake hutoa matunda yake kila wakati:

«أَصْلُهَا ثَابِتٌ وَفَرْعُهَا فِي السَّمَاءِ ۝ تُؤْتِي أُكُلَهَا كُلَّ حِينٍ بِإِذْنِ رَبِّهَا»

“Mizizi yake imethibiti, na matawi yake yako mbinguni. Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake.” [4]

Yeye ndiye mashariki ya nuru za nyota za mbingu ya Wilaya na hazina ya siri za kina za Kitabu cha Uongofu.

Yeye ndiye mke na mama wa viongozi kumi na wawili kutoka katika kizazi cha Ismail (a.s), ambao Mwenyezi Mungu alimweleza Nabii Ibrahim (a.s) habari zao katika sura ya kumi na saba ya kitabu cha Mwanzo (Taurati).

Yeye ndiye alama kuu iliyoonekana mbinguni katika maono ya Yohana; mwanamke aliyejifunika jua, mwezi ukiwa chini ya miguu yake, na kichwani mwake akiwa amevaa taji lenye nyota kumi na mbili. [5]

Yeye ndiye tafsiri ya «Laylatun Mubarakah» (Usiku Uliobarikiwa) katika sura ya Ha-Mim, ambapo ndani yake kila jambo lenye hekima huamuliwa:

«فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ» [6]

“Katika usiku huo kila jambo lenye hekima huamuliwa.”

Yeye ndiye mwanamke pekee aliyetajwa kwa tamko la wingi la kipekee katika Qur’ani Tukufu kupitia neno «نِسَاءَنَا» (wanawake wetu). [7]

Yeye na mume wake ni bahari mbili za Utume na elimu, ambao aya hii imetafsiriwa kuwa inawahusu:

«مَرَجَ الْبَحْرَيْنِ يَلْتَقِيَانِ» [8]

“Anaziendesha bahari mbili zikutane.”

Aya hii imetafsiriwa kuwa inawahusu watu hao wawili. [9]

Katika zama zake, yeye ndiye mwanamke pekee ambaye Mwenyezi Mungu Mtukufu aliifanya dua yake kuwa katika daraja sawa na dua ya Mtume wa Mwisho (s.a.w.w) na Bwana wa Mawasii (a.s), katika siku ya Mubahala.

2. Lulu iliyofichika ya uumbaji

Katika zama zote, Bibi Fatimah (a.s) ndiye mwanamke pekee aliyevaa taji ya kauli ya Mwenyezi Mungu:

«إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللَّهِ لَا نُرِيدُ مِنْكُمْ جَزَاءً وَلَا شُكُورًا» [10]

“Hakika sisi tunakulisheni kwa ajili ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu tu; hatutaki kutoka kwenu malipo wala shukrani.” [11]

Yeye ndiye ambaye Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), katika usiku wa Miiraji, aliona jina lake limeandikwa kwenye mlango wa Pepo kwa maneno haya:

«فَاطِمَةُ خِيَرَةُ اللَّهِ»

“Fatimah ndiye mteule wa Mwenyezi Mungu.” [12]

Ndiyo, Ahmad al-Mukhtar (Mtume Muhammad s.a.w.w) ndiye anayepaswa kuwa na hadhi ya kustahili kuwa pamoja na mwanamke huyo aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu.

Ni yeye ambaye Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema kumhusu:

«أُبْعَثُ عَلَى الْبُرَاقِ خَطْوُهَا عِنْدَ أَقْصَى طَرَفِهَا وَتُبْعَثُ فَاطِمَةُ أَمَامِي»

“Nitafufuliwa nikiwa juu ya Buraq, hatua yake itafika hadi mwisho wa upeo wa macho yangu, na Fatimah atafufuliwa akiwa mbele yangu.” [13]

Inamtosha Bibi Fatimah (a.s) kufufuliwa akiwa mbele ya «Imam wa wa mwanzo na wa mwisho» Siku ya Kiyama, kwani yeye ndiye madhihirisho ya kauli ya Mwenyezi Mungu:

«يَسْعَى نُورُهُمْ بَيْنَ أَيْدِيهِمْ» [14]

“Nuru yao itakuwa ikitangulia mbele yao.”

Hiyo ni nuru inayotangulia mbele ya mtu ambaye atafufuliwa Siku ya Malipo, ambaye Mwenyezi Mungu Mtukufu amemtaja katika Qur’ani Tukufu kwa jina la «Sirajun Munir» (Taa Inayong’arisha), na katika Aya ya Nuru akamfanya kuwa mfano wa nuru Yake.

Katika kueleza utukufu wa Bibi Fatimah (a.s), inatosha kusema kwamba yeye ndiye mtu wa kwanza kuingia katika nafasi ya ukaribu na Mwenyezi Mungu, ambayo imeelezwa kuwa:

«مَقْعَدِ صِدْقٍ عِنْدَ مَلِيكٍ مُقْتَدِرٍ» [15]

“Katika makazi ya kweli mbele ya Mfalme Mwenye uwezo.”

Kama ilivyokuja katika riwaya:

«أَوَّلُ شَخْصٍ يَدْخُلُ الْجَنَّةَ فَاطِمَةُ»

“Mtu wa kwanza kuingia Peponi ni Fatimah.” [16]

Na atakapokaa katika makazi ya rehema ya Mwenyezi Mungu, Manabii wote watakuja kumtembelea:

«زَارَكِ آدَمُ وَمَنْ دُونَهُ مِنَ النَّبِيِّينَ»

“Adam na Manabii wote waliokuja baada yake wamekuzuru.” [17]

Kwa ufupi, vito vilivyofichika katika hazina ya Mwenyezi Mungu Mtukufu vinatokana na chaza ya umaasumu wake. Taa inayong’arisha ya Utume wa Manabii, kuanzia Adam hadi Mtume wa Mwisho, pamoja na mwenge unaong’aa wa Uimamu wa Maimamu waongofu, vyote vinaangazwa na uwepo wa Bibi Fatimah Zahraa (a.s).

Na lulu ya mwisho iliyofichika ndani ya chaza hii, pamoja na nyota yenye kung’aa katika anga hii, ni yule ambaye atajaza ardhi kwa uadilifu na usawa kama ilivyokuwa imejaa dhuluma na ukandamizaji:

«يَمْلَأُ الْأَرْضَ قِسْطًا وَعَدْلًا كَمَا مُلِئَتْ جَوْرًا وَظُلْمًا» [18]


Ataijaza ardhi haki na uadilifu kama ilivyojazwa dhulma na ujeuri

Na kupitia uwepo wake, aya hii itapata tafsiri yake:

«هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَى وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ» [19]

“Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki ili aishindishe dini hiyo juu ya dini zote.”

Na kupitia kudhihiri kwake, aya hii itafasiriwa:

«وَأَشْرَقَتِ الْأَرْضُ بِنُورِ رَبِّهَا» [20]

“Na ardhi itang’aa kwa nuru ya Mola wake.”

3. Laylatul Qadri ya historia

Inapaswa kufahamika kwamba cheo na thamani ya Laylatul Qadri hiyo, ambayo ndiyo mahali pa kuteremka Kitabu Kikuu cha Mwenyezi Mungu, haijulikani kikamilifu. Kadhalika, hadhi ya Kawthar huyo, ambaye ni zawadi kutoka kwa Mola wa Arshi Tukufu kwa Mtume Mtukufu, imefichika mbali na upeo wa ufahamu wetu.

Sheikh Saduq (Mwenyezi Mungu amrehemu) amepokea riwaya katika vitabu vyake vya Al-Amali, Ilal al-Sharai na Al-Khisal kutoka kwa Imam wa Sita, Imam Jaafar al-Sadiq (a.s), kwamba Bibi Fatimah ana majina tisa mbele ya Mwenyezi Mungu (Mwenye nguvu na Mtukufu). Majina hayo ni: Fatimah, Siddiqah, Mubarakah, Tahirah, Zakiyyah, Radiyah, Mardhiyyah, Muhaddathah na Zahraa.

Mwisho wa Hadithi hiyo, Imam alisema:

“Lau Amirul Muuminina (a.s) asingemuoa, basi kusingekuwa na mtu yeyote duniani ambaye angeweza kuwa sawa naye hadi Siku ya Kiyama; kuanzia Adam na kila atakayekuja baada ya Adam.” [21]

Majina hayo ambayo aliyepewa mamlaka ya kuyachagua ni Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu na Mtukufu, kila moja linaashiria daraja na nafasi maalumu ambayo maelezo yake hayawezi kutoshea katika makala hii fupi. Kwa hiyo, tutatosheka na kutaja Hadithi moja kuhusu jina la kwanza.

Imepokewa kutoka kwa Imam wa Sita (a.s) katika tafsiri ya Surat al-Qadr kwamba:

“Laylatul Qadri ni Fatimah, na yeyote atakayemfahamu Fatimah kwa namna inayostahili kumfahamu, basi hakika ameifahamu Laylatul Qadr. Fatimah aliitwa Fatimah kwa sababu viumbe wamekatishwa na kunyimwa uwezo wa kumfahamu.”

Mwanamke ambaye katika utoto wake Mtume wa Mwisho (s.a.w.w) aliamrishwa kufikisha kwake salamu za Mwenyezi Mungu, na Jibril Amin akawa mjumbe wa kuifikisha kwake salamu za rambirambi kutoka kwa Mola wa walimwengu wote, hakika kalamu haiwezi kuandika hadhi yake, wala maelezo ya mwanadamu hayawezi kueleza nafasi yake.

4. Daraja la mtumishi wa mlango wa Bibi Fatimah Zahraa (a.s)

Ibn Shahr Ashub katika kitabu chake cha Manaqib amepokea riwaya kutoka kwa Ali bin Muammar, ambaye alisema:

Baada ya Bibi Fatimah (a.s) kufariki dunia, Ummu Ayman hakuweza kuvumilia kuendelea kuiona sehemu ambayo Siddiqah Kubraa (a.s) alikuwa akiishi mjini Madina. Kwa hiyo, alifunga safari kuelekea Makka. Alipofika katika kituo cha Juhfah, alipatwa na kiu kikali kiasi kwamba akaanza kuhofia maisha yake kutokana na kiu hiyo, aliangalia mbinguni na kusema:

“Ewe Mola wangu! Mimi ni mtumishi wa binti wa Mtume Wako.” Mara hiyo, ndoo ya maji ya Peponi ikateremshwa kwake, akanywa maji hayo na kwa muda wa miaka saba hakuhisi njaa wala kiu. [23]

Ibn Shahr Ashub katika kitabu hicho hicho amepokea riwaya kutoka kwa Malik bin Dinar, ambaye alisema: Wakati watu walipokuwa wakijiandaa kwa ajili ya Hijja, nilimwona mwanamke mmoja akiwa dhaifu na asiye na nguvu. Watu walikuwa wakimshauri aachane na safari hiyo, lakini hakukubali ushauri wao.

Walipokuwa katikati ya jangwa, mnyama aliyekuwa amempanda alishindwa kuendelea na safari. Mwanamke huyo dhaifu aliinua kichwa chake kuelekea mbinguni na kusema: “Hukuniacha nibaki nyumbani kwangu, wala hukuniwezesha kufika katika Nyumba Yako. Lau mtu mwingine yeyote isipokuwa Wewe ndiye angenitendea hivi, ningelalamika kwake mbele Yako.” Ghafla, mtu mmoja alitokea katika jangwa hilo akiwa ameshika hatamu za ngamia-jike. Akamwambia mwanamke huyo: “Panda.” Alipopanda, ngamia-jike huyo alipita katika jangwa hilo kwa kasi ya radi inayong’aa na kupofusha macho.

Nilipofika katika eneo la Tawaf, nilimwona mwanamke huyo akiwa anafanya Tawaf. Nilimwomba kwa kiapo aniambie yeye ni nani, akasema: “Mimi ni Shuhrah, binti wa Maskah, naye ni binti wa Fiddhah, mtumishi wa Bibi Zahraa (a.s).” [24]

Ndiyo, mtu ambaye moyo wake ni Arshi ya Mwingi wa Rehema katika kumtambua Mwenyezi Mungu, ambaye matakwa yake yameyeyuka ndani ya matakwa ya Mwenyezi Mungu, na ambaye miguu yake iliyovimba kutokana na kusimama kwa muda mrefu katika ibada mbele ya Mwenyezi Mungu ni ushahidi wa kujitosa kwake kikamilifu katika ibada ya Mwenyezi Mungu, basi malipo ya kumhudumia yatakuwa ni dua inayojibiwa mbele ya Mola wa mabwana wote.

Aidha, nuru za utukufu wa jua hilo linalong’aa katika anga ya umaasumu ni nyingi zaidi kuliko uwezo wa akili ya mwanadamu kuzielewa. Na yale tuliyoyasema hapa ni ishara fupi tu, ili yawe ukumbusho kwa wenye akili na wenye utambuzi.

Ewe mwenye nyota ya bahati ya juu, uliye siri ya heshima ya Mwenyezi Mungu Mkuu,

Wewe ni binti wa Akili Kuu na mwenza wa Elimu Kuu.

Mapambo ya Arshi ya Mwenyezi Mungu yamelelewa katika paja lako,

Na wewe ni mama wa jua kumi na moja za anga ya maarifa.

Rejea:

[1] Rejea: Jarida maalumu la «Fatimah (a.s); Nukta ya Mabadiliko katika Uumbaji», lililoandaliwa na Kikundi cha Utafiti cha Kituo Maalumu cha Uenezi wa Dini cha Taasisi ya Elimu ya Juu ya Hawza ya Khatam al-Nabiyyin (s.a.w.w), katika siku za Fatimiyyah za mwaka 1399 Hijria Shamsia, ukurasa wa 4.

[2] Furat bin Ibrahim al-Kufi, Tafsir Furat, utafiti: Muhammad al-Kadhim, Wizara ya Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu; Taasisi ya Uchapishaji na Usambazaji, Tehran, mwaka 1410 Hijria Qamaria, ukurasa wa 581.

[3] Rejea: Jarida maalumu la «Fatimah (a.s); Nukta ya Mabadiliko katika Uumbaji», lililoandaliwa na Kikundi cha Utafiti cha Kituo Maalumu cha Uenezi wa Dini cha Taasisi ya Elimu ya Juu ya Hawza ya Khatam al-Nabiyyin (s.a.w.w), katika siku za Fatimiyyah za mwaka 1399 Hijria Shamsia, ukurasa wa 4.

[4] Surat Ibrahim, aya ya 24 na 25.

[5] Maono ya Yohana Mtume, sura ya 12.

[6] “Katika usiku huo kila jambo lenye hekima huamuliwa.” Surat al-Dukhan, aya ya 4. Al-Kulayni, Al-Kafi, Dar al-Kutub al-Islamiyyah, Tehran, mwaka 1365 Hijria Qamaria, juzuu ya 1, ukurasa wa 479.

[7] Surat Aal Imran, aya ya 61.

[8] “Ameziachia bahari mbili zikutane na kuchanganyika.” Surat al-Rahman, aya ya 19.

[9] Sheikh Saduq, Al-Khisal, Machapisho ya Jumuiya ya Walimu wa Hawza, Qum, mwaka 1403 Hijria Qamaria, ukurasa wa 65.

[10] “Hakika sisi tunakulisheni kwa ajili ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu tu; hatutaki kutoka kwenu malipo wala shukrani.” (Surat al-Insan, aya ya 9).

[11] Sheikh Mufid, Al-Irshad, Kongamano la Sheikh Mufid, Qum, mwaka 1413 Hijria Qamaria, juzuu ya 1, ukurasa wa 178.

[12] Al-Khatib al-Baghdadi, Tarikh Baghdad, utafiti: Mustafa Abdul Qadir Ata, Dar al-Kutub al-Ilmiyyah, Beirut, bila kutajwa mwaka wa uchapishaji, juzuu ya 1, ukurasa wa 274.

[13] Maana ya jumla ya kauli hiyo ni kwamba: “Nitafufuliwa nikiwa juu ya Buraq, hatua yake itafika hadi mwisho wa upeo wa macho yangu, na Fatimah atafufuliwa akiwa mbele yangu.” (Al-Hakim al-Naysaburi, Al-Mustadrak Ala al-Sahihayn, utafiti: Mustafa Abdul Qadir Ata, Dar al-Kutub al-Ilmiyyah, chapa ya kwanza, Beirut, mwaka 1411 Hijria Qamaria, juzuu ya 3, ukurasa wa 166).

[14] Surat al-Hadid, aya ya 12.

[15] Surat al-Qamar, aya ya 55.

[16] Al-Dhahabi, Mizan al-I‘tidal, utafiti: Ali Muhammad al-Bajawi, Dar al-Ma‘rifah lil-Tiba‘ah wal-Nashr, Beirut, mwaka 1382 Hijria Qamaria, juzuu ya 2, ukurasa wa 618.

[17] “Adam na Manabii wote waliokuja baada yake watakutembelea.” Tafsir Furat al-Kufi, utafiti: Muhammad al-Kadhim, Wizara ya Utamaduni na Mwongozo wa Kiislamu; Taasisi ya Uchapishaji na Usambazaji, Tehran, mwaka 1410 Hijria Qamaria, ukurasa wa 446.

[18] Sheikh Saduq, Al-Amali, Machapisho ya Maktaba ya Kiislamu, Tehran, mwaka 1362 Hijria Shamsia, ukurasa wa 26, kikao cha 7, Hadithi ya 3.

[19] Surat al-Tawbah, aya ya 33.

[20] Surat al-Zumar, aya ya 69.

[21] Rejea: Al-Amali cha Sheikh Saduq, rejea hiyo hiyo, ukurasa wa 688; Al-Khisal, rejea hiyo hiyo, ukurasa wa 414; Sheikh Saduq, Ilal al-Sharai, Dar al-Murtadha, Beirut, mwaka 1427 Hijria Qamaria, juzuu ya 1–2, ukurasa wa 177.

[22] Tafsir Furat al-Kufi, rejea hiyo hiyo, ukurasa wa 581.

[23] Ibn Shahr Ashub, Manaqib Aal Abi Talib (a.s), Taasisi ya Machapisho ya Allamah, Qum, mwaka 1379 Hijria Qamaria, juzuu ya 3, ukurasa wa 338.

[24] Rejea hiyo hiyo.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha